Ningekuwa mshairi

sanaa

Ningekuwa mshairi, shairi ningetungia
Picha ningeisawiri, ya chombo kinachozama
Ila sina ushairi, wimbo basi takwimbia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Chombo chetu chema chomba, mrama chatuendea
Rubani kafanye jambo, tusije kuangamia
Kwa mawimbi yalo kombo, ya dhiki na ya tanzia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Kila siku ni mitutu, mitutu ya haramia
Pasina chembe cha utu, vizazi kuangamia
Zimepiga nyoyo kutu, zisijali kuumia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Umekaa kwenye basi, au kwako watulia
Unakufika mkosi, mauti kukufikia
La kujuta hulikosi, kilio kulialia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Kilio ndo letu vazi, wana chombo abiria
Mazishi kwetu si kazi, kazi hasa ni kulia
Uchungu ulio wazi, “ni nini?” twaulizia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Wageni wametokoma, maisha wakihofia
Ushuru ukatukoma, hohehahe twajutia
Magazetini twasoma, uchumi wadidimia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Mayatima na wajane, kila siku wazidia
Na chombo kisongamane, vilema wanaumia
Usiku hadi manane, twahofu wa kuvamia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Yalianza vipi yote, haya yakatufikia
Milungula kotekote, waovu wakaingia
Pia mali yetu sote, wachache wakabugia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Ubaguzi wa rubani, na walomzingiria
“Huyu mwana wa fulani, mpe kazi naridhia”
Lonyimwa wakalaani, kajiunga haramia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Rubani haambiliki, msimamo atetea
Na wazidi kufariki, wanyonge maabiria
“Makiwa” za kinafiki, kila kutwa twasikia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Chombo kimekuwa huru, sasa miaka nusu mia
Furaha yetu ni nduru, mikosi kujivunia
Hakuna la kushukuru, chombo kukisafiria
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Muhimu ni tuungane, wenye chombo abiria
Tukae tusemezane, suluhu itatujia
Tukisema tulumbane, adui anasikia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Tamati natamatisha, na dua kwake Jalia
Bahari inatutisha, tunusuru tunalia
Bandari kutufikisha, kwa salama salimia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.