Ningekuwa mshairi

sanaa

Ningekuwa mshairi, shairi ningetungia
Picha ningeisawiri, ya chombo kinachozama
Ila sina ushairi, wimbo basi takwimbia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Chombo chetu chema chomba, mrama chatuendea
Rubani kafanye jambo, tusije kuangamia
Kwa mawimbi yalo kombo, ya dhiki na ya tanzia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Kila siku ni mitutu, mitutu ya haramia
Pasina chembe cha utu, vizazi kuangamia
Zimepiga nyoyo kutu, zisijali kuumia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Umekaa kwenye basi, au kwako watulia
Unakufika mkosi, mauti kukufikia
La kujuta hulikosi, kilio kulialia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Kilio ndo letu vazi, wana chombo abiria
Mazishi kwetu si kazi, kazi hasa ni kulia
Uchungu ulio wazi, “ni nini?” twaulizia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Wageni wametokoma, maisha wakihofia
Ushuru ukatukoma, hohehahe twajutia
Magazetini twasoma, uchumi wadidimia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Mayatima na wajane, kila siku wazidia
Na chombo kisongamane, vilema wanaumia
Usiku hadi manane, twahofu wa kuvamia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Yalianza vipi yote, haya yakatufikia
Milungula kotekote, waovu wakaingia
Pia mali yetu sote, wachache wakabugia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Ubaguzi wa rubani, na walomzingiria
“Huyu mwana wa fulani, mpe kazi naridhia”
Lonyimwa wakalaani, kajiunga haramia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Rubani haambiliki, msimamo atetea
Na wazidi kufariki, wanyonge maabiria
“Makiwa” za kinafiki, kila kutwa twasikia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Chombo kimekuwa huru, sasa miaka nusu mia
Furaha yetu ni nduru, mikosi kujivunia
Hakuna la kushukuru, chombo kukisafiria
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Muhimu ni tuungane, wenye chombo abiria
Tukae tusemezane, suluhu itatujia
Tukisema tulumbane, adui anasikia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.
Tamati natamatisha, na dua kwake Jalia
Bahari inatutisha, tunusuru tunalia
Bandari kutufikisha, kwa salama salimia
Mshairi ningetunga, ya chombo kinachozama.

ZAMZAM

Ewe wangu zamzama, mrembo mwenye nidhama
Pokea zangu salama, lizopima kwa mizama
Ndipo utulie mama, kama maji zamzama
Ewe wangu Zamzama, Amekuumba Karima

Ewe wangu mwana mwali, meno meupe ya wail
Mwenye sifa za jamali, bila shaka wala swali
Sura imekukubali, akhera tangu awali
Ewe wangu Zamzama, Amekuunda Kamali

Ewe wangu wa moyoni, niweke mwako rohoni
Wenginewe siwaoni, hawanifiki machoni
Tangu tuwe utotoni, hadi siku za usoni
Ewe wangu Zamzama, Amekutunga Manani

Ewe wangu mwenye wema, thabiti usotetema
Wa vitendo na kusema, tabia iso kilema
Mtiifu wa mapema, sifa zako ninasema
Ewe wangu Zamzama, Amekuchonga Rahima

Ewe wangu wa harusi usiyejua matusi
Usothamini fulusi, ulobobea durusi
Naomba ino ruhusi nikusifu kwa kirusi
Ewe wangu Zamzama, Amekuunga Kudusi

Ewe wangu wa milele, usiyependa kelele
Usiyefanya kejele, wala fujo za kengele
Nitakuenzi milele, kaburini hata mbele
Ewe wangu Zamzama, Amekhulonga Nyasaye

Ewe wangu wa fahari, wa mambo nzima bahari
Kifua chako habari, na kiuno machachari
Wa maungo yenye ari, yalo nguvu za ghubari
Ewe wangu Zamzama, Amekutanda Jabari

Ewe wangu wa nadhifa, usafi ni yako sifa
Nimezuru mataifa, huna wa yako sharifa
Unazua taarifa, ajabu kimataifa
Ewe wangu Zamzama, Amekujenga Latifa

Ewe wangu zamzama, basi kwako ninazama
Nomba uje nitazama, kwa pendo la kila zama
Bila wewe naungama pweke zitaniandama
Ewe wangu Zamzama, Amekuumba Rahima

Itikia

Una nini hunioni, nambile kilo machoni

Pengine miye mshoni, nikushone na usoni

Ole wa zangu fashoni, hazipiti zako mboni

Funguka lango rohoni, nione mwangu moyoni

Unione!

 

Una nini huelewi, uwe kama hutendewi

Bidii sizichelewi, nakulewesha hulewi

Unelezwa huelewi, wazo halipokelewi

Basi nasema sipewi, kwa fahamu siendewi

Unelewe!

 

Una wapi hunijii, pangu katu hujitii

Pangu pano hufikii, na roho huyachilii

Ongea usinidhii, nije hapo kwa bidii

Fanyile karama hii, nijile sikukimbii

Unijile!

 

Una nini hunihisi, hisia za kihalisi

Burudaniyo rahisi, kunichuja zako hisi

Una ngumu taasisi, ja jiwe kikuakisi

Basi pata tashihisi, uhai sijifilisi

Unihisi!

 

Dhiki si kitu kizuri, kwangu ni kama kaburi

Hazina wema uturi, hunizaba kwa kiburi

Ila zako za suduri, zanikata furifuri

Kangamsha yangu nuri, itikia niwe huri

Itikia!